Mmoja wa wanamgambo wa Al Shabaab wanaosemekana kuuawa kwa shambulizi la Westgate
Picha za wanajeshi wa Kenya
waliokwenda katika jumba la Westgate katika juhudi za uokozi na kisha
baadaye kuonekena kwenye kamera za CCTV wakiondoka na mifuko ya
plasitiki yenye bidhaa za madukani, bila shaka zimewashangaza wengi.
Picha hizo mwanzo zimeonyesha wanajeshi
wakiingia ndani ya jengo hilo wakiwa wamebeba silaha kukabiliana na
wanamgambo walioshambulia jengo hilo wiki nne zilizopita na baadaye
wakitoka wakiwa wamebeba mifuko hiyo wakiwa na silaha zao kwa wakati
mmoja.
Hata hivyo haijulikani walichokuwa wamekibeba kwenye mifuko hiyo .
Pamoja na picha za wanajeshi wakiwa wamebeba
mifuko, pia kulikuwa na picha zengine zilizoonyesha mashine ya pesa
zikiwa zimeporwa ndani ya mikahawa huku picha za alama za risasi kwenye
maeneo ya kuhifadhia pesa, pia zikionekana.
Inaarifiwa ilikuwa jaribio ya kufungua hifadhi hizo ambalo halikufanikiwa.
Madai haya ya wanajeshi kufanya uporaji wa
maduka katika jingo hilo, yalikanushwa vikali na jeshi la Kenya kiasi
cha kutaka hatua kuchukuliwa dhidi ya waliokuwa wanatoa madai hayo,
lakini haijulikani jibu lao litakuwa nini hasa kwa picha hizo za CCTV
zilizoonyesha wanajeshi hao wakifanya uporaji.
Wamiliki wa maduka waliorejea kwenye maduka yao
bbaada ya shambulizi , walidai kuwa maduka yao yaliporwa ingawa jeshi
lilikanusha madai hayo baadhi ya taarifa zikisema kuwa ilikuwa njama ya
wafanyabiashara kudai fidia kwa mali zao zilizoharibika.
Sio wanajeshi pekee waliotuhumiwa kwa uporaji,
kwani polisi mmoja naye alifikishwa mahakamani kwa kosa la uporaji baada
ya kupatikana na pochi la mtu liliokuwa na damu.
Wangambao wa Al Shabaab waliteka nyara jengo la
Westgate kwa siku nne na kusababisha vifo vya watu 60 pamoja na
kuwajeruhi zaidi ya watu miamoja.